Maambukizi ya Covid-19 yanapenyenza katika kaunti zilizo nje ya zile zilizofungwa

Mwenyekiti wa kamati ya afya ya baraza la magavana Profesa Anyang’ Nyong’o, ameonya kwamba kaunti zilizo nje ya zile zilizofungwa kutokana na idadi kubwa ya visa vya maambukizi ya COVID-19, zimeanza kunakili ongezeko la visa vya ugonjwa huo.

Akisema kuwa hali hiyo inatokana na maambukizi ya kijamii, Prof. Nyong’o alizihimiza kaunti zote kuzingatia kanuni za wizara ya afya, zikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji, kuvalia barakoa katika maeneo ya umma, na kutokaribiana.

Hata hivyo alisema kuwa kaunti zimejiandaa ipasavyo kushughulikia ongezeko lolote la visa vya maambukizi ya COVID-19, akisema kwamba kaunti 32 zimeongeza idadi ya vitanda katika muda wa juma moja lililopita.

Prof. Nyong’o, alisema kuwa serikali za kaunti zinatekeleza hatua za kuhakikisha kwamba watu wanaolengwa katika awamu ya kwanza wanapata chanjo katika kipindi kilichowekwa.

Aliihimiza wizara ya afya kuongeza idadi ya vipimo vinavyosambazwa, ili kutimiza lengo hilo na kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Wakati huo huo, Profesa Nyong’o alisema kuwa usambazaji wa mapato kwa kaunti, umesalia kuwa changamoto, kwani wizara ya afya imetoa shilingi bilioni-19.8, huku wizara hiyo ikiwa bado haijatoa shilingi bilioni-66.

Aliihimiza wizara ya fedha kutoa pesa hizo, ili kuziwezesha serikali za kaunti kuendeleza shughuli zake na kulipa bili, kwa wawasilishaji bidhaa na huduma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *