Maafisa wa DCI wamwokoa mwanaume aliyetekwa nyara Mombasa
Maafisa wa Idara ya upelelezi kuhusu Uhalifu mnamo Jumamosi alfajiri walimwokoa mtu mmoja ambaye alikuwa ametekwa nyara katika eneo la Changamwe, Kaunti ya Mombasa.
Kulingana na idara hiyo kwa mjibu wa ujumbe katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Wambua Mutuku mwenye umri wa miaka 26 ana bahati ya kusherehekea Siku Kuu ya Utamaduni na familia yake baada ya wapelelezi hao kumuokoa kutoka kwenye genge lililokuwa limejihami kwa panga.
Idara hiyo ilisema mmoja wa wanachama wa genge hilo aliuawa kwa kupigwa risasi wakati wa shughuli ya uokoaji huo huku washirika wake wakitoroka eneo hilo.
Panga tano na silaha zingine butu zilipatikana katika eneo la uhalifu.
Mutuku alikuwa ametekwa nyara na kupelekwa eneo la Lilongwe huko Mombasa, ambapo maafisa wa upelelezi na maafisa wa Polisi waliwapata watekaji nyara hao na wakamuokoa.