Maafisa 11 wa usimamizi mtihani wakamatwa kwa udanganyifu

Maafisa 11 wa usimamizi wa mtihani wamekamatwa katika kipindi cha juma moja lililopita, kwa kufungua karatasi za mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne-KCSE, kabla ya wakati kamili wa kufungua.

Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano, waziri wa elimu profesa George Magoha, alisema maafisa hao wanahusisha wasimamizi wa vituo na wale wa mtihani kutoka kaunti za Homa Bay, Mandera, Kisii, Garissa na Kisumu.

Profesa Magoha pia alisema kwamba kwa sasa wanawasaka maafisa waliowafungulia baadhi ya wanafunzi karatasi ya kwanza ya somo la masuala ya kilimo.

Hata hivyo waziri huyo alilihakikishia taifa hili kwamba jaribio hilo halijaathiri uadilifu wa mtihani huo kwani karatasi zilizofunguliwa hazikuwa zimeonekana na wanafunzi.

Alisema karatasi zilizosalia zimehifadhiwa vyema ili kuhakikisha uadilifu wa mtihani huo.

Alimuonya mtu yeyote anayenuia kujihusisha na udanganyifu kwamba kwamba ataadhibiwa vikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *