Lucy Maino apoteza taji ya Miss Papua New Guinea kwa kucheza densi

Mwanadada huyo mzaliwa wa taifa la Papua New Guinea alivishwa taji hiyo mwaka 2019 baada ya kushinda shindano la ulimwende nchini humo.

Ameendelea kushikilia nafasi hiyo kwa zaidi ya mwaka mmoja kutokana na janga la Corona ambalo limesababisha mikutano ifutiliwe mbali katika sehemu nyingi ulimwenguni.

Muda mfupi baada ya kupachika video hiyo kwenye akaunti yake ya Tik Tok, wengi walimkosoa wakisema haifai kutoka kwa mtu anayetizamiwa na mabinti wa umri mdogo na watu wengine nchini humo.

Alifuta video hiyo baadaye lakini kuna watu ambao tayari walikuwa wameipata na wakaisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Kamati ya shirika linalosimamia shindano la ulimbwende nchini Papua New Guinea, yaani Miss Pacific Islands Pageant PNG (MPIP PNG) ilitangaza kwamba Bi. Lucy Maino amepokonywa taji kuanzia wiki hii.

Huku wengi wakimkashifu, wengine wanahisi kwamba ameonewa sana kiasi ya kupokonywa taji yake. Allan Bird, Gavana wa eneo la Sepik Mashariki ambaye pia ni mwenyekiti wa kundi la wabunge dhidi ya dhulma za kijinsia alikemea hatua ya wengi kuzomea Lucy kwenye mitandao ya kijamii akishangaa ni jamii gani inakosoa mauaji na mateso dhidi ya wanawake na inakasirishwa pia na video ya mwanamke akipiga densi.

Mwanadada ambaye aliwahi kushikilia taji ya Miss Papua New Guinea ambaye hakutaka kutajwa alisema kitendo dhidi ya Lucy ni cha unyanyasaji akisema ingekuwa ni mwanaume wengi wangekuwa wanamshangilia.

Bi. Maino ni mchezaji hodari wa mpira wa miguu na kwa sababu hiyo alipata usaidizi wa masomo katika chuo kikuu cha Hawaii ambapo alisomea shahada ya Usimamizi wa Biashara.

Mwaka 2019, aliwakilisha Papua New Guinea kama nahodha msaidizi wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ambapo walishinda nishani mbili za dhahabu katika michezo ya Pacific huko Apia, Samoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *