LSK kupinga kanuni za usalama kuhusu maandalizi ya mikutano

Rais wa Chama cha Wanasheria humu nchini LSK Nelson Havi ametangaza nia ya chama hicho kupinga mahakamani kanuni kali zilizotolewa na baraza la ushauri kuhusu usalama wa kitaifa, kuhusu maandalizi ya mikutano ya hadhara.

Havi ambaye alikuwa akizungumza mtaani Kibra wakati wa maadhimisho ya siku ya Huduma alisema hatua hiyo ni dhihirisho la mazoea ya ukiukaji sheria kwani kanuni hizo hazina msingi katika sheria.

Mnamo Alhamisi, Baraza la Mawaziri liliidhinisha kanuni hizo za kudhibiti maandalizi ya mikutano ya hadhara, jinsi vyombo vya Habari vinavyopaswa kuangazia matukio na jumbe zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Akitangaza maagizo hayo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Joseph Kinyua alisema mwanasiasa yeyote anayepania kuandaa mkutano wa hadhara ni sharti amjulishe afisa msimamizi wa kituo cha polisi (OCS) kati ya siku 3 hadi 14 kabla ya mkutano huo.

Wanasiasa husika watatakiwa kuhudhuria mikutano hiyo na kuwasaidia polisi kulinda usalama kwa kuhakikisha uzingatiaji wa maagizo yatakayotolewa na OCS.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *