Lil Wayne akabiliwa na tishio la kufungwa jela

Mwanamuziki wa Marekani wa mtindo wa rap Dwayne Michael Carter Jr maarufu kama Lil Wayne huenda akahukumiwa kifungo cha hadi miaka kumi gerezani kwa kosa la kupatikana na silaha hata baada yake kushtakiwa kwa kosa sawia awali.

Haya yalibainika jumanne katika mahakama moja ya Florida.

Tarehe 23 mwezi Disemba mwaka 2019 polisi walifanya msako kwenye ndege ya kibinafsi ya mwanamuziki huyo na kupata bastola na risasi kwenye mizigo yake. Alipatikana pia na dawa za kulevya ila hajashtakiwa kwa hilo.

Polisi hao pia waliripoti kwamba Wayne alionekana mlevi kutokana na jinsi alikuwa akizungumza na kushindwa kufungua macho vizuri wakati wa msako huo wa mwaka jana.

Wakili wa Lil Wayne Howard Srebnick hata hivyo amethibitisha kwamba mwanamuziki huyo hajakamatwa na hakujatolewa maagizo ya kumtia mbaroni. Kulingana naye hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba mteja wake alikuwa ananuia kutumia silaha hiyo.

Wayne naye alijitetea akisema bastola hiyo ilikuwa zawadi aliyokabidhiwa kwenye siku ya kusherehekea kina baba ulimwenguni. Wayne anatarajiwa kufika mahakamani tareje 11 mwezi Disemba mwaka huu.

Yapata miaka kumi iliyopita, Lil Wayne alishtakiwa huko New York kwa kosa la silaha na akafungwa jela kwa muda wa miezi nane. Sheria ya Amerika, inazuia wakosaji kumiliki silaha.

Siku chache kabla ya uchaguzi wa Urais nchini Marekani, Lil Wayne alijitokeza na kuunga mkono Rais Donald Trump hatua ambayo ilisababisha mpenzi wake ambaye ni mwanamitindo kwa jina Denise Bodot amuache.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *