Likizo ya Mapenzi!

Huu ndio msamiati mpya nchini Tanzania kwa sasa na unatokana na usemi wa mama mzazi wa msanii Ali Kiba.

Mama huyo alikuwa akihojiwa katika kituo cha redio cha Clouds nchini Tanzania ambako alifichua kwamba mke wa Ali kwa jina Amina Khalef yuko nyumbani alikozaliwa Mombasa Kenya kwa ajili ya likizo ya ndoa ama ukipenda mapenzi.

Hili ni dhibitisho kwamba ndoa yao bado ipo kinyume na minong’ono kwamba walisha achana.

Ndoa ya Ali Kiba na mwanadada huyo wa Kenya imekuwa ya misukosuko mingi na mara nyingi huwa inatokea kwamba yuko nyumbani kwao nchini Kenya. Msanii Ali Kiba huwa hapendi kuzungumzia jambo hilo kwenye mahojiano ila analokubali ni kwamba hakuna ndoa ambayo haina matatizo.

Wakati wa mahojiano hayo, mamake Ali Kiba alifichua mengi kuhusu familia yake. Alisema Ali Kiba ndiye kifungua mimba wake na kuna wengine watatu.

Kuna wa pili Abdul kareem ambaye pia ni mwanamuziki kwa jina Abdu Kiba, akifuatiwa na binti wa pekee Zabibu na kitinda mimba ni Abubakar Swadik ambaye ni mpiga picha wa Ali Kiba.

Jina Kiba alisema ni ufupi wa jina “Kibanio” ambalo lilikuwa jina la utani la baba ya watoto wake ila jina halisi la baba Ali Kiba ni “Ng’ang’ise”.

Kulingana naye Ali alianza kuhisi na kupenda muziki akiwa na umri wa siku saba tu. Alipata tatizo mwanzo kukubali kazi ya mwanawe kama mwanamuziki aliyekuwa akiimba nyimbo za kidunia lakini baadaye ilibidi akubali.

Mama Ali Kiba amehudhuria maonyesho yake ya muziki kama mara tatu tu kwa nia ya kujua kinaoendelea humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *