Kurejelewa kwa safari za ndege kati ya Kenya na Tanzania kutaimarisha utalii baina ya nchi hizo

Baraza la kibiashara la kanda ya Afrika mashariki limesifu hatua ya serikali za Kenya na Tanzania ya kuafikiana wakisema itafanikisha kurejelewa kwa safari za ndege kutoka Kenya hadi Tanzania.

Baraza hilo limepongeza halmashauri ya uchukuzi wa ndege nchini Tanzania na ile ya Kenya kwa kufanikisha makubaliano hayo kuhusu kurejelewa kwa huduma za uchukuzi wa ndege katika kanda ya Afrika mashariki.  

Baraza hilo lilisema kuwa hatua hiyo itaimarisha utalii katika kanda hii, biashara baina ya nchi za kanda hii na biashara baina ya Kenya na Tanzania na hivyo kuwezesha ufufuzi wa kibiashara na kiuchumi.

Kwenye taarifa afisa mkuu wa baraza hilo Dr. Peter Mathuki alisema kuwa kufunguliwa kwa anga baina ya nchi hizi majirani kutawezesha kuongezeka kwa huduma za uchukuzi wa ndege, kurahisisha usafiri wa watu na kufanikisha usafirishaji wa bidhaa.

Vile vile alisema kufunguliwa huko kwa safari za ndege, kutafungua soko kubwa zaidi na kuimarisha utalii katika kanda hii.

Dr. Mathuki wakati huo huo alizihimiza nchi washirika wa jumuiya ya Afrika mashariki kutafakari kufutilia mbali ada za uingizaji bidhaa, kupunguza ushuru wa forodhani wa mafuta ya ndege, uegeshaji na ada zinazohusiana na janga la COVID-19.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *