Kura ya maamuzi yanukia huku kaunti zikiendelea kupitisha BBI

Siku ya Jumanne huenda ikaamua mwelekeo wa mchakato wa marekebisho ya katiba humu nchini, huku mabunge kumi ya kaunti yakitarajiwa kuidhinisha mswada wa marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Mabunge ya Kaunti za Narok, Makueni na Machakos yamesema yako tayari kuunga mkono mswada huo utakapowasilishwa siku hiyo na hivyo kuongeza uwezekano kwamba hitaji la kikatiba la kuwa na angalau kaunti 24 zilizouithibisha mswada huo litatimizwa.

Bunge la Kaunti ya Samburu ndilo la hivi punde kupitisha mswada huo na kufikisha 12, jumla ya kaunti zilizopitisha mswada huo.

Kaunti hizo ni pamoja na Siaya, Homabay, Kisumu, Busia, Pokot Magharibi, Trans Nzoia, Kajiado, Kisii, Vihiga, Nairobi, na Laikipia, huku Baringo ikisalia kaunti ya pekee kukatalia mbali mswada huo.

Hivi leo Gavana wa Kaunti ya Makueni Kivutha Kibwana ameonekana kubadili msimamo akisema ataunga mkono mchakato huo n ahata kuwahimiza wawakilishi wadi wa kaunti hiyo kufuata mkondo huo.

Mabunge ya kaunti kadhaa za eneo la Mlima Kenya yanatarajiwa kujadili mswada huo Jumanne, unaohitaji kuungwa mkono na angalau mabunge 12 zaidi ili kutoa fursa ya marekebisho ya katiba.

Kaunti zengine zinazotarajiwa kujadili mswada huo wiki hii ni Tharaka Nithi, Nakuru, Nyeri, Embu, Murang’a, Migori, Bungoma, Kakamega na Taita Taveta.

Awali, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga alikuwa alisema ana imani kwamba kufikia Jumanne wiki hii, mswada huo utakuwa umeungwa mkono na idadi ya kaunti zinazohitajika kikatiba.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *