Kundi la waendeshaji pikipiki Meru latoa msaada wa visodo kwa wasichana

Kundi la waendeshaji pikipiki linalofahamika kama Meru Passionate Riders limezindua mpango wa kufanya kampeni ya kutoa visodo kwa wasichana katika eneo la Mugae, kwenye mpaka wa Kaunti ya Meru na Isiolo.

Mwenyekiti wa kundi hilo Koome Kinyua amesema mpango huo ulizinduliwa kutokana na haja iliyopo ya kuwasaidia na kuwalinda wasichana kutoka familia maskini ili wasinyanyaswe kimapenzi na wanaume kwa ubadilishanaji na visodo.

“Tulifanya hivi kwa sababu ya zile changamoto ambazo wasichana wa Mugae wanapitia ambapo mzee anamwambia mtoto alale naye kwanza ndio amnunulie visodo,” amesema Kinyua.

Mpango huo unashirikiana na ule wa Tujijenge Mashinani, kundi la Straight Talk na shirika la Africa Research Services ambazo zilitoa mavazi ya ndani kwa wasichana na wavulana.

Casty Mucheni, Mkurugenzi wa mpango wa Tujijenge Mashinani amesema mradi huo pia huandaa mashauriano ya kuwapa vijana uwezo.

“Watoto 200 watafaidika na visodo na nguo za ndani ambazo tumeleta leo,” akasema Mucheni.

Naibu Chifu wa sehemu hiyo Peter Gitile Mikwa amesema visa vya wasichana kutungwa mimba katika sehemu hiyo vinazua wasiwasi.

Amelipongeza kundi hilo kwa kuongoza juhudi za mpango huo wa kutoa ushauri nasaha ambapo vijana na wasichana wa sehemu hiyo pia hupokea mafunzo kuhusu maadili.

Amesifu mpango huo ambao amesema unasaidia hasa wakati huu ambapo wanafunzi wamekuwa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na athari za janga la ugonjwa wa COVID-19 ambazo zimesababisha kufungwa kwa shule.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *