Kundi la vijana Nakuru lazindua mpango wa kunyunyizia kemikali taasisi za umma

Huku athari za janga la Corona zikiendelea kushuhudiwa kote nchini, kundi la vijana wataalamu kutoka Eneo Bunge la Bahati limezindua mpango wa kunyunyizia kemikali za kuua virusi vya Corona katika taasisi za umma.

Mpango huo unaolenga shule 60 za umma, vituo vitatu vya afya na masoko matatu pia unanuia kuwahamasisha wakazi wa eneo hilo kuhusu kanuni za Wizara ya Afya za kuzuia maambukizi.

Kulingana na kiongozi wa kundi hilo Samuel Kimani Murage, mpango huo utakaodumu kwa muda wa miezi sita pia utajumuisha kutoa msaada wa vifaa vya kujikinga kama vile sabuni, barakoa, kwa familia zisizojiweza.

Akiongea katika eneo la Mawanga baada ya shughuli ya kunyunyizia kemikali Shule ya Upili ya Workers, Murage amesema mpango huo unaosimamiwa na maafisa wa afya ya umma, unakusanya michango ya fedha kutoka kwa watu mbali mbali zinazosaidia kutekeleza shughuli za kundi hilo katika juhudi za kupunguza kiwango cha maambukizi ya COVID-19 katika Kaunti ya Nakuru.

Kupitia misaada ya wahisani, kundi hilo limeweza kununua vifaa vya unyunyiziaji na kemikali za kuua virusi vya Corona.

Murage amesema kuwa hiyo ni njia moja ya kudhihirisha nafasi ya vijana katika vita dhidi ya janga la Corona ambalo limelemaza uchumi, kusababisha vifo na kuwaacha maelfu wakiendelea kupokea matibabu baada ya kuambukizwa ugonjwa huo.

Amewahimiza vijana kote nchini kushirikiana na maafisa wa afya ya umma katika maeneo yao katika kuendeleza juhudi za kupambana na janga hilo ambalo amelilaumu kwa kuwaacha vijana wengi bila kipato.

Kauli yake imeungwa mkono na wanachama wengine wa kundi hilo, Wangui Njoroge, Steve Mwangi na Kariuki Thumi, ambao wamesema ni jukumu lao kuwa sehemu ya suluhu ya matatizo yaliyosababishwa na janga hilo.

Wizara ya Afya humu nchini imeitaja Kaunti ya Nakuru kuwa moja ya sehemu zinazopaswa kuangaziwa zaidi kufuatia ongezeko kubwa la visa vinavyoripotiwa vya ugonjwa wa COVID-19 katika muda wa miezi miwili iliyopita.

Mpango huo unajiri wiki chache baada ya wanafunzi 68 na walimu watano katika Shule ya Upili ya Wasichana na Bahati kuthibitishwa kuambukizwa COVID-19, hali ambayo imezua hofu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *