Kukamatwa kwa ‘Bobi Wine’ nchini Uganda kwa sababisha maafa ya watu watatu

Maafisa wa polisi nchini Uganda wanasema watu watatu waliaga dunia  na wengine kadhaa kujeruhiwa jijini Kampala na katika miji mingine baada ya mwaniaji Urais, Robert Kyagulanyi, al-maarufu Bobi Wine, kukamatwa wakati wa mkutano wa kampeni.

Taarifa ya polisi hata hivyo haikueleza jinsi watu hao walivyoaga dunia.

Picha na video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha waathiriwa wakiwa wamelala chini wakiwa wameloa damu huku ikionekana kana kwamba walipigwa risasi.

Ghasia zilizuka jijini Kampala kufuatia maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwa Bobi Wine anayezuiliwa Wilayani L’uuka’ baada ya polisi kumshutumu kwa kuandaa mkutano wa hadhara kinyume cha maagizo ya wizara ya afya ya kuzuia kusambaa kwa Korona.

Mwaniaji mwingine, Patrick Amuriat Oboi, pia amekamatwa.

Kwingineko mwaniaji urais nchini Uganda Mugisha Muntu amesitisha shughuli zake za kampeni hadi wawaniaji urais wa upinzani waliokamatwa siku ya Jumatano watakapoachiliwa huru.

Muntu ametoa wito wa kuachiliwa huru kwa Robert Kyangulanyi almaarufu Bobi wine na Patrick Amuriat ambao walikamatwa katika shughuli tofauti za kampeni.

Uchaguzi wa Urais utaandaliwa nchini Uganda mwezi Januari mwakani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *