KLM Azindua Video ‘Mungu Saidia’ Akisema Ukombozi wa Afrika ni Sasa Hivi

Mwanzo wa wikii hii Msanii wa Hiphop Kaa la Moto (KLM) alizindua video ijulikanayo kama ‘Mungu Saidia’. Ingawa video hiyo iliyotayarishwa na Qamah ni mpya, wimbo huo ni moja ya zile zilizopo kwenye ‘Kesi’, albamu aliyochapisha Julai mwaka wa 2019.

Sauti nyororo inayorembesha ‘Mungu Saidia’ ni ya malkia Vivonce msanii chipukizi.

Kwenye ‘Mungu Saidia’ KLM anapasa sauti mambo yanavyoenda mrama na anauliza Karima maswali tata kama vile mbona demokrasia imekua ‘demogasia’? Je, tofauti kati ya upangaji uzazi na uvyaaji mimba ipi? Mbona wana wa viongozi wa kidini wamekua malaya? Kwa nini vita dhidi ya ugaidi vinazidi kuwa biashara? Tutamaliza vipi tamaa ya nchi za Afrika kukopa nchi za mashariki na magharibi? Kwa nini maskini hawaagi uchochole?

Akizungumzia uongozi, anastajabika kama nuksi ya Ronald Ngala ya ukarimu ndio kizuizi katika kuongeza ushawishi wa viongozi kutoka ufuo wa Pwani nchini na kunufaisha maisha ya wakaazi.

Historia ya Kenya inanukuu Ronald Ngala na Oginga Odinga walisusia madaraka wakisema lazima Rais Jomo Kenyatta, Bildad Kagia, Ramogi Achieng Onek, Paul Ngei, Fred Kubai na Kungu Karumba wangeachiliwa kwanza kutoka korokoroni huko Kapenguria kati ya mwaka wa 1952 na 1953.

KLM anakanusha kwamba video ya ‘Mungu Naomba’ ilichelewa. Anatukumbusha mwaka wa 2020 kulikuwa na virusi vya Corona ambavyo vilimfanya azingatie uuzaji wa albamu ya ‘Kesi’ kote ulimwenguni.

Albamu ya ‘Kesi’ ilitayarishwa na NJE wa Ufuoni Records, Sango wa Malinda Records, Okoth Oyiera na Teknixx. Usafishaji ulifanywa na gwiji wa muziki wa Hiphop Chizn Brain ambaye makao yake kwa muda ni Dar es Salaam, Tanzania.

Video zingine zilizofanya kutoka kwa albamu ya ‘Kesi’ ni ‘Msafiri’ na ‘Kenda’ na uchoraji kwenye gwanda ilifanywa na Ciro G.

Mwisho wa mwaka jana hadi sasa KLM ameshirikishwa kwa video zingine kama ‘Jua’ akiwa na Viquee na Fikra Teule wa Angaza Zetu, kikundi kikali cha hiphop cha hapo awali kutoka Mombasa; na ‘Last Warriors’ iliyowaleta pamoja wasanii kutoka Afrika Mashariki ikiongozwa na Kikosi Kazi, Trabolee, Trabolee, Kayvo Kforce na Romi Swahili.

Kaa la Moto. Picha/Hisani

‘Last Warriors’ ni tunda la mjadala kati ya KLM na Azma wa Kikosi Kazi cha Tanzania. Ilifaa kuwaleta wasanii wa kizazi cha tatu, lakini KLM aliwatafuta wanamashairi wa kizazi cha nne kwani baadhi yao wanazingatia uandishi nasaha. Xtatic, Scar na Smallz Lethal wangeshiriki lakini walikuwa nje ya Nairobi kwa sababu ya shughuli muhimu za kibinafsi.

KLM anasisitiza ‘Last Warrior’ ni hatua ya kwanza sio kuwaleta tu wasanii wa Afrika Mashariki pamoja bali Afrika nzima. Miaka ishirini iliyopita, Kenya ilikuwa na kikundi cha hiphop kiitwacho Ukoo Flani Maumau kilicholeta pamoja Ukoo Flani kutoka Mombasa; Kalamashaka, Wenyeji, Wakamba Wawili, MC Kah na Mashifta kutoka Nairobi; na Dee7 kutoka Tanzania. Miaka ya tisini nchini Tanzania kulikuwa na Kwanza Unit kilichojumulisha Villain Gangsters, Riders Posse na Tribe-X na kilichangia sana ukuaji wa tasnia ya hiphop katika nchi hiyo.

KLM anatumai Afrika itakuwa moja hivi karibuni na anasihi kila Mwafrika ajihusishe kwa undani kwenye swala hili. Anawahimiza vijana kusoma zaidi historia sahihi ya Afrika ili kuelewa bara linatoka wapi na linaelekea wapi.

Charlotte O’Neal aka Mama C akiwa Arusha, Tanzania. Picha/Hisani

Mwanzo wa mwaka wa 2021, KLM alikuwa Tanzania kuipigia debe albamu ya ‘Kesi’ na pia kushiriki kwenye tamasha kadhaa. Pia alimtembelea huko Arusha mwanaharakati wa wa Umoja wa Africa na Black Panther Party Charlotte Hill O’Neal (Mama C). KLM anakiri kuwa Mama C ambaye pia ni mke wa Pete O’Neal mwanachama wa Black Panther hujenga taswira zake za ukombozi wa Afrika kutoka kwa ukoloni mamboleo.

Akizungumzia mwaka wa 2021, anasema wafuasi wake watarajie mema na kuongeza kuwa “mimi sio msanii wa kutoa ngoma kila siku, mimi natoa kazi zinazowagusa wote kila siku”. Kulingana na KLM, albamu ya ‘Kesi’ iliuzwa sana mwaka wa 2019 na 2020.

KLM anasisitiza hiphop ni salama na inazidi kunawiri kwa kasi nchini Kenya na Bara la Afrika. “Hiphop ingekuwa imekwisha hatungekuwepo – pia vipengee vyake kama breakdance, uana dj, na kufoka vinakuwa”, alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *