Kisumu All Stars kumenyana na Vihiga United Fc kuwania kucheza ligi kuu FKF

Timu ya 18 na ya mwisho kushiriki ligi kuu ya FKF itabainika Jumatano Novemba 4 wakati wa kuchezwa kwa mkondo wa pili wa fainali ya mchujo baina ya Kisumu All Stars dhidi ya Vihiga United katika uwanja wa Moi Kaunti ya Kisumu.

All Stars wanaongoza mabao 2-1 kutokana na awamu ya kwanza Jumamosi iliyopita ,huku wakilenga kusalia ligini baada ya kumaliza katika nafasi ya 16 msimu jana  na watahitaji tu sare katika pambano hilo la jumatano ili kuafikia malengo yao.

Kwa upande wao Vihiga United walimaliza katika nafasi ya 3 katika ligi ya Nsl na wanahitaji ushindi wa mabao 2-0 katika mchuano wa marudio ili kurejea ligini tangu washushwe daraja kutoka ligi kuu mwaka 2018.

All stars ndiyo timu pekee kutoka eneo la Nyanza iliyokuwa ikishiriki ligi kuu msimu jana ,na inafadhiliwa na serikali ya kaunti ya Kisumu.

Msimu wa mwaka 2020-2021 wa ligi kuu utang’oa nanga tarehe 20 mwezi huu na kukamilika mei mwaka ujao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *