Kipindi kuhusu Nameless na Wahu

Wanamuziki hawa wawili wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka kama 15 hivi na ndoa yao ni mojawapo ya zile za watu maarufu ambazo zimesimama wima.

Na sasa wameamua kusimulia kuhusu uhusiano wao kupitia “This Love” kipindi ambacho kitakuwa kikipatikana kwenye jukwaa la mitandaoni kwa jina “Showmax”.

“This Love” ni jina la mradi fulani wa muziki ambao walifanya kila mmoja kivyake kabla ya kutoa kibao “Te Amo” kwa pamoja.

Kulingana na taarifa ya Showmax Kenya, kipindi hicho kimegawanywa kwa sehemu 13 na kinaangazia maswala tofauti kama vile mapenzi, maisha, historia na waliyojifunza kwenye familia na katika muziki.

Haya yanajiri wakati ambapo wapenzi hawa wanaandaa albamu yao ya kwanza pamoja.

Wanatizamia kwa furaha kazi hiyo ambapo wataweza kuonyesha mashabiki wao ubunifu unaoingia kwenye kazi hiyo, changamoto za kufanya kazi pamoja na vile vile uzuri wa kufanya kazi pamoja.

Wanaosaidia kufanikisha kazi yao pia watajulikanishwa kwa umma.

Wanapoadhimisha miaka 20 kwenye ulingo wa muziki nchini Kenya, wanadhamiria pia kuonyesha mambo ambayo wamejiifunza wakijaribu kutimiza majukumu yao kama wanandoa, wazazi na washirika wa biashara.

Hiki sio kipindi cha kwanza kinachoangazia maisha ya watu maarufu nchini Kenya. Mwanamuziki Bahati aliwahi kuwa na chake kwa jina “Being Bahati” na wanandoa Dj Mo na Size 8 wakawa na chao kwa jina “Dine with the Murayas”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *