Kinoti: Polisi hawashirikiani na wahalifu kuwahangaisha wakenya

Mkurugenzi wa idara ya upelelezi wa uhalifu wa jinai, George Kinoti, amekanusha madai kwamba polisi wanashirikiana na wahalifu kuwahangaisha Wakenya.

Akijibu kipindi kilichopeperushwa katika kituo kimoja cha habari humu nchini, Kinoti alisema ripoti hiyo ilionekana kuwa na nia mbaya ya kufedhehesha huduma ya taifa ya polisi.

Alisema ripoti hiyo haikutayarishwa vyema huku wale walioitayarisha wakiamua kuangazia visa vichache kulaumu huduma yote ya taifa ya polisi.

Mkurugenzi huyo aliongea katika makao makuu ya idara ya upelelezi ambako wanahabari walionyeshwa bunduki moja iliyopambuliwa ambayo ilikuwa imesalimishwa.

Watalam wa bunduki waligundua kwamba bunduki aina ya AK 47 ambayo ilinunuliwa haikuwa ya huduma ya taifa ya polisi bali aina ya bunduki ambazo hutumika mara nyingi na wahalifu katika visa vya wizi wa mifugo na ujambazi.

Idara ya upelelezi pia imesema kuwa haijawahi kuona aina ya bastola ndogo ambayo inaaminika kutengenezwa nchini Uturuki ambayo pia ilisalimishwa kwa polisi.

Wataalam wa bunduki waliokuwa kwenye mkutano huo wa kuwaarifu wanahabari walisema nambari za usajili wa silaha hizo hazifanani na zile serikali imetoa.

Kinoti aliwataka wanahabari kuwahusisha maafisa wa usalama wanapotayarisha ripoti kama hizo, akisistiza kwamba kuna utaratibu wenye uwajibikaji katika huduma ya taifa ya polisi wa kuhakikisha silaha hazimilikiwi na wahalifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *