Kibao kipya cha Ringtone

Awali picha zilisambazwa kwenye mitando ya kijamii zikionyesha mwanamuziki Ringtone akitiwa mbaroni na ripoti kwamba alikamatwa kwa ajili ya dhulma za kingono.

Hayo hayakuwa kweli kwani sasa imefahamika kwamba picha hizo zilikuwa za sehemu ya igizo kwenye video ya wimbo wake mpya unaoitwa “Backslide” ambao amemshirikisha mwimbaji wa Tanzania Martha Mwaipaja.

Kwenye maigizo ya video ya wimbo huo, Ringtone analeta taswira ya kusingiziwa kuwa mbakaji na dada ambaye alikuwa amemsaidia kwa kumpa lifti kwa gari lake akisema hata baada ya kusingiziwa hawezi kurudi nyuma katika safari yake kama mkristo.

Kibao hiki kimezinduliwa wakati kuna tetesi kwamba Ringtone aliwahi kumdhulumu kimapenzi mfanyibiashara Bridget Achieng.

Bridget alichukua hatua ya kuelezea tukio hilo kupitia video mubashara akisema wakati huo hakuwa anajiweza na alipokutana na Ringtone ambaye alikuwa amekwenda kutumbuiza chuoni mwao akaahidi kumsaidia kurekodi muziki wake.

Kulingana na mama huyo wa mtoto mmoja, Studio ya Ringtone ilikuwa nyumbani kwake na alipofika Ringtone aliamua kumtendea unyama hata kabla ya kurekodi muziki.

Achieng anasema alijaribu wakati huo kuripoti Ringtone kwa polisi lakini hakufanikiwa.

Baada ya tetesi hizo kuvuja, Ringtone naye alichapisha video akijitetea kutokana na madai hayo isijulikane kama ulikuwa mpango wa wawili hao wa kutayarisha mashabiki kwa kazi mpya ambayo Ringtone ameitoa leo kwenye You Tube.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *