Kesi ya ufisadi dhidi ya Jacob Zuma kuanza mwezi Mei

Mahakama moja ya Afrika kusini imesema kuwa kesi ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma na kampuni moja ya ulinzi ya Ufaransa Thales kuhusiana na mkataba wa kununua silaha wa zaidi ya dola bilioni mbili inaanza mwezi Mei.

Zuma anakabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ufujaji na ulanguzi wa pesa ambayo ameyakanusha yote.

Zuma anadaiwa kupokea kinyume cha sheria malipo ya kila mwaka kutoka kampuni ya Thales baada ya kuafikiana kuhusiana na maswala ya silaha mwaka wa 1999.

Zuma alitwaa wadhifa wa naibu wa Rais nchini Afrika kusini mwaka wa 1999 na kutwaa urais mwongo mmoja baadaye.

Mshauri wake wa kifedha Schabir Shaikh alipatikana na hatia ya kujaribu kuitisha hongo kutoka kwa kampuni hiyo ya Ufaransa na kufungwa jela mwaka wa 2005. 

Kesi dhidi ya Zuma ilitupiliwa mbali pindi tu baada yake kuwania urais mwaka wa 2009. 

Hata hivyo siku ya Jumanne, mahakama kuu ya Pietermaritzburg imesema kuwa kesi hiyo itaanza kusikizwa tena tarehe 17 mwezi Mei mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *