Kenya yaripoti idadi kubwa zaidi ya waliopona COVID-19 huku wengine 321 wakiambukizwa

Kenya leo imenakili idadi kubwa zaidi ya watu waliopona korona kwa siku moja tangu kuthibitishwa kwa kisa cha kwanza cha ugonjwa huo hapa nchini mwezi Machi mwaka huu.

Wagonjwa 4,328 wamepona ambapo 4,222 walikuwa chini ya mpango wa utunzi wa nyumbani, ilhali 106 waliruhusiwa kuondoka katika vituo mbali mbali vya afya nchini.

Hata hivyo nchi hii imethibitisha visa vipya 321 vya maambukizi na kuongeza idadi jumla ya maambukizi humu nchini hadi 39,907.

Visa hivyo vilitokana na sampuli 4,342 zilizopimwa. Kwa sasa jumla ya sampuli zilizopimwa ni 569,678.

Kwenye taarifa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema kati ya visa hivyo vipya, 309 ni Wakenya ilhali 12 ni raia wa kigeni.

183 ni wanaume ilhali 138 ni wanawake,huku mwathiriwa wa umri mdogo akiwa mtoto wa miezi tisa na umri mkubwa miaka 88.

Kaunti ya Nairobi imeendelea kuongoza kwa visa vingi zaidi, 109, ikifuatwa na Nakuru 37, Trans Nzoia 32, Mombasa 31, Kisumu 16, Narok 16, Kisii 15, Uasin Gishu 12, Meru 9, Kilifi 8, Kiambu 7, Siaya 5, Laikipia 5, Kajiado 4, Kericho 3, Machakos 2, Migori 2, huku Bomet, Homabay, Kitui, Lamu, Marsabit, Nandi, Nyandarua na Tharaka-Nithi zikiripoti kisa kimoja kila moja.

Hata hivyo watu watano zaidi wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo na kuongeza idadi jumla ya vifo kutokana na COVID-19 humu nchini hadi 748.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *