Kenya yajitosa katika jitihada za kutafuta chanjo dhidi ya Covid-19

Kenya imejiunga na jitihada za ulimwengu za  kutafuta chanjo  dhidi ya ugonjwa wa COVID-19, huku majaribio ya chanjo hiyo kwa jina  ChAdOx1 nCoV-19  yakianza.

Kwenye taarifa, taasisi ya utafiti wa dawa nchini  KEMRI, imesema kundi la kufanya majaribio ya chanjo hiyo tayari imewachanja watu wa kwanza waliojitolea kufanyiwa majaribio baada ya kupata idhini ya kuendelea na majaribio.

Chanjo hiyo itawalenga watu 40 ambao wako katika mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa huo katika kaunti ya Kilifi.

Ikiwa chanjo hiyo itadhibitishwa kuwa salama, watu wengine 360 waliojitolea pia watajumuishwa kwenye utafiti huo kutoka kaunti ya Mombasa.

Baada ya chanjo hiyo, waliohusishwa watafanyiwa uchunguzi kwa muda wa miezi 12 kukadiria afya yao na dalili zozote za madhara ya chanjo hiyo.

Uchunguzi huo unanuia kutathmini ikiwa chanjo hiyo ya  ChAdOx1 nCoV-19 ni salama , na ikiwa italeta kinga mwilini kwa watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *