Kenya yaipiga kumbo Sudan na kutinga nusu fainali Cecafa
Timu ya taifa ya Kenya kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 20, imefuzu kwa nusu fainali ya michuano ya Cecafa inayoendelea mjini Arusha
Tanzania, baada ya kuilaza Sudan mabao 2-1 katika pambano la mwisho la kundi C uwanjani Sheikh Amri Abeid .
Baada ya kipindi cha kwanza kumalizikia kwa sare tasa ,Fortune Omoto aliondoa ukame wa mabao kwa bao la dakika ya 62 kwa Kenya , lakini zikisalia dakika tano mechi ikatike Ali Gozoli Nooh akavunja nyoyo za wakenya kwa bao kusawazisha .
Hata hivyo Benson Ochieng alipachika bao la dakika ya 92 na kuhakisha Kenya maarufu kama rising stars ,wanamaliza kwenye nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 6 kutokana na mechi mbili na kufuzu kwa nusu fainali ya Jumatatu dhidi ya Hippos kutoka Uganda huku Tanzania walioongoza kundi A wakiweka miadi ya kumenyana na Sudan kusini katika nusu fainali ya pili pia Jumatatu.

Timu ya kwanza na ya pili katika michuano hiyo ambayo fainali yake itapigwa Disemba 2 zitafuzu kushiriki mashindano ya kombe la Afcon kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka ujao nchini Mauritania.
Rising Stars walikuwa wamesajili ushindi wa mabao 3-0 katika mechi ya kwanza ya kundi hilo dhidi ya Ethiopia.