Categories
Michezo

Kenya yailemea Sudan katika mechi ya kirafiki

Timu ya Kenya kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 maarufu kama Rising Stars,  ilikuwa na wakati mgumu kabla ya kuishinda Sudan mabao 2-1 katika mchuano wa kujipima nguvu uliochezwa Alhamisi jioni katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Kenya walianza kwa uzembe huku Sudan walichukua uongozi katika dakika ya 4 kabla ya mshambulizi  Brian Wanyama kusawazisha  wenyeji kunako dakika ya 35.

Licha ya mashambulizi kutoka kwa pande zote kipindi cha kwanza kilimalizika kwa sare ya bao 1-1 .

Wachezaji wa Kenya wakimiliki Mpira  Uwanjani Nyayo                        picha @Mnyamwezi

Katika kipindi cha pili  timu zote zilicheza kwa tahadhari kubwa lakini utepetevu wa Sudan katika dakika ya 78 kulimpa  Matthew Mwendwa  nafasi ya kupachika bao la ushindi  kwa Rising Stars.

Ulikuwa ushindi wa pili kwa Kenya dhidi ya Sudan baada ya kuwapiga mabao 3-1 tarehe 2 mwezi huu katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani katika pambano jingine la kirafiki.

Kenya chini ya ukufunzi wa Stanley Okumbi sasa wanajipanga kuelekea Arusha Tanzania kushiriki mashindano ya CECAFA baina ya Novemba 22 na Desemba 6 ambapo wamejumuishwa kundi C pamoja na Ethiopia na Sudan.

Risinga Stars wakisherehekea bao                                                                                picha @Mnyamwezi

Kundi A linajumuisha mabingwa watetezi na wenyeji  Tanzania, Rwanda, Somalia, na  Djibouti, wakati kundi B likiwa na  Burundi, Eritrea, South Sudan na Uganda.

Timu bora kutoka kila kundi pamoja na timu bora ya pili kutoka makundi yote matatu ,zitafuzu kwa nusu fainali huku timu mbili zitakazotinga fainali zikifuzu kwa mashindano ya Afcon mwaka ujao.

Rising Stars walipoteza bao 1-0 kwa Serengeti Boys ya Tanzania katika fainali ya mwaka jana ya CECAFA  nchini Uganda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *