Kenya yahitaji shilingi bilioni 6.2 kupambana na mabadiliko ya anga

Rais Uhuru Kenyatta amesema Kenya inahitaji takriban shilingi bilioni 6.2 kutekeleza hatua za kujinusuru kutokana na mabadiliko ya hali ya angaa kwa lengo la kupunguza kiwachngo cha uchafuzi wa mazingira kwa asili mia 32.

Rais amesema hayo kupitia njia ya video wakati wa maadhimisho ya tano ya mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya hali ya anga ambayo pia yalishuhudia kukamilika kwa mkataba wa Kyoto.

Kiongozi wa taifa amesema Kenya imejitolea kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kiwango cha asilimia 30 na kwamba serikali itafadhili juhudi hizo kwa kitita cha shilingi bilioni 1.24, huku ufadhili uliosalia wa bilioni 4.96 ukitolewa na jamii ya kimataifa.

Rais Kenyatta amesema Kenya inashuhudia athari kadhaa za mabadiliko ya hali ya anga ikiwemo ukame wa kila mara pamoja na mvua kubwa inayogharimu nchi hii asilimia tatu ya pato lake la jumla kila mwaka.

Rais amesema Kenya imejitolea kufufua uchumi wake baada ya janga la ugonjwa wa COVID-19 kwa kuhakikisha kwamba sekta tofauti za kiuchumi zinastahimili athari za mabadiliko ya hali ya anga.

Ameongeza kuwa Kenya ni miongoni mwa mataifa ya kwanza ya Kiafrika kuweka mikakati ya muda mrefu kuzuia uchafuzi wa hali ya anga kuambatana na makubaliano ya Paris.

Rais ametoa wito kwa mataifa ya kundi la kiuchumi la G20 pamoja na mashirika makubwa kujitolea kuzuia uchafuzi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *