Kenya U 17 yafurushwa CECAFA na kukosa fursa ya kufuzu AFCON
Kenya ilitmuliwa kwenye michuano ya Cecafa na kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kombe la AFCON kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17 mjini Rubavu Rwanda.
Vijana wa Kenya walitarajia Uganda ambao ni mabingwa watetezi waishinde Ethiopia mabao 6-0 siku ya Ijumaa katika pamano la mwisho la kundi A ili watinge nusu fainali baada ya Kenya kunyukwa mabao 5-0 na Uganda katika mechi ya ufunguzi.

Uganda iliwacharaza Ethiopia mabao 3-0 katika mechi ya mwisho iliyochezwa Ijumaa katika uwanja wa Umuganda na kuongoza kwa pointi 6 wakifuatwa na Ethiopia kwa alama 1 huku Kenya pia ikisha mkia kwa alama 1.
Haya ni mashindano ya pili mtawalia ambayo Kenya imekosa fursa ya kushiriki michuano ya Afcon mwakani baada ya timu ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 pia kuibuka ya nne katika mashindano ya Cecafa yaliyokamilika Tanzania mapema mwezi huu.
Mashindano hayo ya CECAFA yanayoshirikisha mataifa 6 yataingia nusu fainali Jumapili Uganda wakifungua ratiba dhidi ya Djibouiti kabla ya Tanzania kumaliza udhia Ethiopia.
Fainali ya kipute hicho kupigwa Disemba 22 huku timu ya kwanza na ya pili zikifuzu kushiriki mashindano ya Afcon mwezi Juni mwakani nchini Moroko.