Kenya kunufaika na Akademia ya ndondi na ukumbi wa mazoezi kutoka AIBA

Mabondia wa humu nchini watanufaika na akademia ya ndondi na ukumbi wa mazoezi  utakaojengwa katika uwanja wa Kasarani na shirikisho la ndondi duniani AIBA.

Akizungumza  jijini Nairobi  baada ya kuongoza kikao kupitia mtandaoni na viongozi wa mashirikisho ya ngumi Afrika,Rais wa AIBA Umar Kremlev alisema kuwa akademia hiyo na ukumbi wa kisasa wa mazoezi vitajengwa kwa gharama ya AIBA huku shughuli hiyo ikitarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Mchango wetu tutahakikisha gym hiyo,akademia  zimefunguliwa ,tutajenga pamoja na kufungua  kwa kutumia pesa zetu na ikiwezekana kabla ya mwisho wa mwaka huu,tunaomba wakandarasi watakaopewa kazi hiyo wasituhujumu”akasema

Kremlev  kutoka Urusi ,ameongeza kuwa ujenzi wa akademia hiyo na ukumbi wa mazoezi utakuwa wa kwanza Afrika kabla ya kutekeleza miradi sawa na hiyo katika mataifa mengine ya Afrika ikiwemo Moroko na Uganda.

Naye Rais wa shirikisho la ndondi Afrika Dkt Mohammed Moustashane  ameipongeza ziara ya Rais Umar barani Afrika huku pia akielezea matumaini yake kuwa bara hili litanyakua angaa medali tatu kwenye michezo ya Olimpiki ya mwaka huu baina ya Julai na Agosti mjini Tokyo Japan.

“Nichukue fursa hii kumshukuru Rais  Umar kwa kuzuru Afrika kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe na mipango ya miradi ya maendeleo aliyo nayo kwa bara hili,nina imani kuwa mabondia wa Afrika watazoa angaa medali tatu katika michezo ya Olimpiki ya mwaka huu kutokana na muda wa matayarisho mwingi ambao wamekuwa nao tangu mashindano ya kufuzu mapema mwaka jana “akasema Dkt Moustashane

Kinara wa shirikisho la masumbwi nchini kenya Athony Ombok Jamal alimpongeza kiongozi huyo wa AIBA nchini  na kusema kuwa atakutana na viongozi kutoka wizara ya michezo baadae wiki hii ili kukamilisha mikakati ya ujenzi wa akademia na ukumbi wa mazoezi uwanjani Kasarani.

“Ninafurahia sana ziara ya Rais ambaye ametuletea mazuri na kuwa taifa la kwanza Afrika kwake kuzuru ,hii haijawahitokea nitakutana na viongozi kutoka wizara ya michezo mapema wiki hii ili kuhakikisha ujenzi na shughuli yote inatekelezwa”akasema Jamal

Katika ziara yake ya siku mbili jijini Nairobi Umar aliongoza kikao na viongozi wote wa mashirikisho ya masumbwi Afrika.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *