Kenya iko mbioni kufanya majaribio ya chanjo dhidi ya COVID-19

Majaribio ya chanjo ya Oxford dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 humu nchini yameingia hatua ya tatu, huku uwezo na usalama wa chanjo hiyo ukitarajiwa kujulikana mwishoni mwa mwezi huu.

Kenya iliungana na mataifa mengine ulimwenguni katika harakati ya kutafuta chanjo ya COVID-19 na kufanyia majaribio chanjo aina ya ChAdOx1 nCoV-19.

Majaribio hayo yanaendeshwa na shirika la KEMRI-Wellcome Trust, tawi la Kilifi kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Oxford na Shirika la Wellcome Trust nchini Wingereza.

Ikiwa majaribio ya chanjo hiyo yataonyesha uwezo wa zaidi ya asilimia 90 ya kukinga na hatimaye kuidhinishwa na Shirika la Afya Duniani, Kenya itakuwa miongoni mwa nchi zitakazosifika kwa kupiga hatua kwenye vita dhidi ya janga la ugonjwa huo.

KEMRI sasa imefanya majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu baada ya kupata idhini kutoka kwa Wizara ya Afya na Serikali ya Kaunti ya Kilifi.

Wahudumu wa afya 40 wa serikali ya Kaunti ya Kilifi walijitolea kwa majaribio hayo.

Ikiwa usalama wa chanjo hiyo utathibitishwa, watu wengine 360 watasajiliwa kwa majaribio hayo yatakayopanuliwa hadi katika Kaunti ya Mombasa.

Chanjo hiyo inadaiwa kuongeza kinga kwa watu wenye umri wa miaka 60 na 70, hali inayoleta matumaini kwamba kundi hilo lililo kwenye hatari pia linaweza kupata kinga dhidi ya virusi vya Corona.

Chanjo hiyo ya ChAdOx1 nCoV-19 imetengenezwa na Chuo Kikuu ya Oxford kwa ushirikiano na Kampuni ya AstraZeneca na inafanyiwa uchunguzi katika mataifa mbali mbali yakiwemo Wingereza, Afrika Kusini na Brazil.

Kufikia sasa, aina tatu za chanjo, Pfizer-BioNTech, Sputnik na Moderna, zimeripotiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kukinga dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 baada ya kufanyiwa majaribio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *