Juliani na chama cha Jubilee wazozania hakimiliki

Mwanamuziki Juliani kwa jina halisi Julius Owino Ooko ameshtumu chama cha Jubilee kwa kile anachokitaja kuwa kukiuka hakimiliki yake kwa kutumia wimbo wake kwa jina “Utawala” kutangaza mpango wa maridhiano nchini BBI bila idhini yake.

Siku ya mwisho ya mwezi Oktoba, Juliani aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba rafiki zake walikuwa wamemtumia video hiyo ambapo wimbo wake umetumika bila idhini.

Tarehe mosi mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 mwanamuziki huyo aliandika tena kwenye akaunti yake ya Twitter akielezea kwamba hakuna yeyote kutoka chama tawala cha Jubilee ambaye alikuwa amejibu madai yake au kutaka kuzungumzia swala hilo.

“Mpaka sasa no one from @JubileePartyK ame reach out ku explain hii mambo. Niko rada yao. I didn’t licence this,” ndiyo maneno aliandika Juliani.

Wengi wa wafuasi wake na wanamuziki wenza walionekana kumhimiza achukue hatua za kisheria kuhusu swala hilo.

Kennedy Ombima au ukipenda King Kaka alimwandikia, “Tayari wameanza kutumia vijana na bado BBI haijaanza. Pesa kwenye benki!”

Nonini naye alishangaa ni nani anayefanya jambo kama hilo hadi sasa na kuhimiza hakimiliki iheshimiwe nchini Kenya.

Baada ya hapo Juliani alichapisha picha za barua ya wakili wake kwa chama cha Jubilee kupitia kwa katibu mkuu Raphael Tuju, ambayo inakitaka chama hicho kufuta video hiyo mara moja na kukubali kosa la kukiuka hakimiliki kwa muda wa saa 72 ili wasikilizane jinsi ya kulipia hilo.

Wakili huyo anaendelea kueleza kwamba ikiwa hayo hayatatekelezwa, mteja wao amewapa idhini ya kuanzisha kesi mahakamani.

Wakili huyo anasema mteja wake Juliani huwa hana mwegemeo kwa upande wowote wa kisiasa nchini na wimbo wake kwa jina “Utawala” ulinuiwa tu kukosoa usimamizi wa nchi.

“Utumizi wa Wimbo huo na chama cha Jubilee huenda ukaharibia mwanamuziki Juliani kazi siku za usoni kwa kumwonyesha kuwa anayepigia upatu upande fulani wa siasa na kuingilia kazi yake siku za usoni.” ndiyo baadhi ya maneno kwenye barua hiyo ya wakili.

Chama cha Jubilee hakijajibu madai hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *