Joho awataka viongozi wasioridhika na chama cha ODM wahame

Naibu wa kiongozi wa chama cha ODM Hassan Ali Joho amewadiriki viongozi wa Pwani ambao hawaridhiki na uongozi wa chama hicho kukihama na kutafuta kura kupitia vyama vingine.

Joho ameshutumu baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka sehemu hiyo ambao wanapigania kubuniwa kwa chama kipya, ambacho wanadai kitapigania maslahi ya Wapwani.

Gavana huyo wa Mombasa amewataja viongozi hao kuwa wadanganyifu na wenye nia ya kujitafutia riziki kupitia utapeli.

Amesema kubuniwa kwa chama kipya kutawagawanya zaidi Wapwani na kuhujumu umoja katika sehemu hiyo ambao umedumishwa na chama cha ODM.

Joho amesema kuwa tangu Rais Uhuru Kenyata na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walipoungana kwa ajili ya kuleta umoja, miradi kadhaa ambayo itaboresha maisha ya wakazi wa sehemu ya Pwani imeanzishwa na serikali kuu.

“Kama naibu wa kiongozi wa chama cha ODM ambaye nimeona sehemu ya Pwani ikifaidika kwa miradi ya maendeleo tangu Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga waungane, naweza kusema bila tashwishi kwamba adui mkubwa wa maendeleo ya Pwani ni [Naibu Rais William] Ruto na wale wanaokula kutoka sahani lake, ambao sasa wanadai kutaka kuunda chama,” amesema Joho.

Gavana huyo amesema eneo la Pwani linatarajiwa kupata ufadhili zaidi wa kifedha kupitia ugatuzi na kubuniwa kwa hazina za maendeleo ya Wadi, ikiwa mpango wa BBI utaidhinishwa kupitia kura ya maamuzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *