Jisafishe bila kumtaja Ruto, Duale amkanya Kalonzo

Aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale amemkanya Kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka dhidi ya kuliingiza jina la Naibu Rais William Ruto kwenye kesi yake ya umiliki wa ardhi ya Yatta.

Kalonzo alijisalimisha kwa Idara ya Upelelezi wa Uhalifu (DCI) kufuatia matamshi ya Ruto kwamba kipande chake cha ardhi cha Yatta ni mali ya serikali.

Aidha, kundi la wanasheria likiongozwa na Seneta wa Kaunti ya Siaya James Orengo waliwasilisha kesi kadhaa dhidi ya Naibu Rais kufuatia matamshi yake.

Lakini Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale anasema Kalonzo anastahili kujisafisha kutokana na madai hayo bila kumhusisha Ruto katika kesi hiyo.

“Kama uko na kesi na DCI kuhusu ardhi ya NYS na unataka kusafisha jina lako, tunashangaa jinsi William Ruto anavyohusika hapo, nenda ukajitetee kama Kalonzo,” amesema Duale.

Duale amesema hayo alipokuwa akitoa msaada wa vitu mbali mbali kwa wahasiriwa wa mkasa wa moto uliotokea wiki mbili zilizopita.

Mbunge huyo ameongeza kuwa uhusiano pekee uliopo kati ya Ruto na Kalonzo ni kwamba wote wawili wako katika kinyang’anyiro cha safari ya ikulu katika uchaguzi mkuu ujao.

Wiki iliyopita, Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na Naibu Rais William Ruto walirushiana madai ya unyakuzi wa ardhi.

Hii ni baada ya Ruto kudai kwamba Kalonzo alijipatia ardhi hiyo ya Yatta kwa njia isiyokuwa halali, huku Kalonzo naye akidai kwamba Ruto ametajwa kwenye kesi kadhaa za unyakuzi wa ardhi humu nchini.

Baada ya Kalonzo kujiwasilisha kwenye Idara ya DCI, alimpa changamoto Ruto pia afuate mkondo huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *