Jeshi la Nigeria lakana kuwaua waandamanaji

Jeshi la Nigeria limekanusha madai kuwa liliwaua waandamanaji wasio na silaha kwenye mkutano jijini Lagos mnamo mwezi uliopita.

Wanajeshi hao wamedai kuwa walikuwa wakitumia bunduki ambazo hazikuwa na risasi kwenye makabiliano na raia.

Afisa mmoja mkuu, Brigedia Jenerali Ahmed Taiwo aliwasilisha ushahidi wa kanda ya video kuthibitisha madai yake yaliyotolewa kwa jopo la wachunguzi.

Shirika la Kimataifa la kutetea haki, Amnesty International linasema watu 12 waliuawa wanajeshi walipofyatua risasi wakati wa maandamano ya kupinga ukatili wa polisi katika mtaa wa mabwenyenye wa Lekki, jijini Lagos.

Walioshuhudia waliliambia Shirika la Utangazaji la BBC kuwa wanajeshi waliwafatulia waandamanaji risasi.

Waandamanaji wengine 1,000 walikuwa wamekusanyika kwenye lango la kukusanya ushuru katika barabara ya kueleke mtaa wa Lekki mnamo tarehe 20 Oktoba kuzuia magari kutumia barabara hiyo kuu.

Askari waliripotiwa kuonekana kuweka vizuizi katika barabara ya kuelekea eneo la maandamano muda mfupi kabla ya risasi kuanza kufyatuliwa.

Shambulizi hilo lilitokea baada ya siku kadhaa za maandamano dhidi ya kitengo cha polisi cha Kupambana na Ujambazi, SARS, ambacho mienendo ya maafisa imekashifiwa vikalina na raia wa nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *