Jay Z aingilia biashara ya mazoezi ya mwili

Mwanamuziki wa nchi ya Marekani wa mtindo rap Jay Z anaonekana kufuata nyayo za mke wake Beyonce katika biashara ambapo naye sasa ameingilia biashara inayohusiana na michezo na mazoezi.

Jay Z amewekeza kwenye mashine mbili za mazoezi ambazo mtu huwa ni kama ambaye anakwea kwa lengo la kuimarisha viungo vya mwili na hasa mgongo.

Mwanamuziki huyo anaungana na mchezaji tenisi tajika Novak Djokovic kwenye biashara hiyo ya mashine za mazoezi kwa jina CLMBR ambazo bado hazijazinduliwa rasmi.

Wawili hao wamezisifia mashine hizo wakisema zitabadili mambo kwenye mazoezi ya mwili. Mashine hiyo ina skrini ambapo mtumiaji ataweza kufuatilia maagizo ya kocha katika kuitumia kwenye mazoezi na kuafikia matokeo bora.

Haya yanajiri muda mfupi baada ya Beyonce kutia saini mkataba na kampuni kwa jina Peloton ambapo atatumika kuonyesha mitindo mbali mbali ya mazoezi ya mwili. Peloton ni kampuni ya vifaa vya mazoezi na pia huwa inaunda video ya mazoezi ya mwili.

Beyonce pia aliingilia biashara ya mavazi ya michezo au mazoezi ambayo pia yanaweza kuvaliwa mtu akiwa mapumzikoni au wakati wowote.

Wanandoa hao wawili wanaonekana kushirikiana katika biashara ambapo Beyonce alizindua rasmi albamu yake kwa jina Lemonade, kwenye jukwaa la mtandaoni kwa jina “Tidal” linalomilikiwa na mume wake.

Binti yao Blue Ivy pia hajaachwa nyuma, akiwa na umri wa miaka 8 tu, amesharekodi muziki na kushinda tuzo za BET. Mamake amemshirikisha pia katika mauzaji ya mavazi yake ya michezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *