Jamii ya wakanamungu yajitolea kusaidia Jemutai

Jamii ya wakanamungu nchini Kenya imejitolea kusaidia mchekeshaji Jemutai ambaye hivi maajuzi alitikisa mitandao ya kijamii kwa kufichua kwamba ameshindwa kugharamia watoto wake na kufichua baba ya watoto hao.

Kwanza, alianza kwa kumwomba Edgar Obare amtafutie mnunuzi wa akaunti yake ya Facebook ili aweze kulipa kodi ya nyumba na kujikimu kimaisha.

Hapo ndipo aliamua kumwaga mtama kuhusu uhusiano wake na mchekeshaji mwenza Proffesor Hamo ambaye ametelekeza watoto wao na hatimizi majukumu yake kama baba mzazi.

Kupitia mitandao ya kijamii, shirika hilo la wakanamungu maarufu kama “Atheists In Kenya Society” lilitoa taarifa kwamba litasaidia mchekeshaji Jemutai kulipa kodi ya nyumba.

Taarifa hiyo ambayo imetiwa saini na Harrison Mumia ambaye ni kiongozi wa kundi hilo, inamsihi Jemutai awasiliane nao haraka iwezekanavyo ili apokee usaidizi huo.

Mumia anaendelea kusihi serikali kuanzisha hazina ya kusaidia kina mama ambao wanalea watoto peke yao huku akiomba kanisa na bodi ya kuorodhesha filamu nchini KFCB pia zisaidie wasanii ambao wanateseka kutokana na janga la Corona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *