Jamii ya Turkana yalalamikia kudhulumiwa na maafisa wa Polisi

Watu wa jamii ya Turkana wanaoishi katika Kaunti ya Isiolo wamelalamikia dhuluma zinazotekelezwa na maafisa wa polisi huko Daaba na baadhi ya sehemu za wodi ya Ngaremara.

Polisi wanatekeleza msako katika sehemu hiyo dhidi ya wahalifu walioshambulia maafisa wa GSU kutoka Kituo cha Polisi cha Mariara huko Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru  pamoja na maafisa wa polisi wa kukabiliana na wizi wa mifugo kutoka Bullu majuma mawili yaliopita.

Wakiongea katika Kijiji cha Emejen, wakazi wa sehemu hiyo wakiongozwa na  Martin Miriti pamoja na Augustine Elimlim wamedai kwamba maafisa hao wanaadhibu jamii yote ya Waturkana katika sehemu ya Ngaremara kutokana na uovu unaotekelezwa na wachache.

Huku wakishtumu kitendo cha kushambuliwa kwa maafisa wa polisi, wakazi hao pia wamewahimiza maafisa hao kuwasaka wahalifu halisi badala ya kuwadhulumu wasio na hatia.

Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Herman Shambi hata hivyo amekanusha madai kwamba polisi wanatumia nguvu kupita kiasi kwenye msako huo.

Wiki iliyopita, wakazi wa Ngaremara walisalimisha bunduki kumi haramu kwa kamishna huyo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *