Jamii ya Ogiek yadai kubaguliwa katika usajili wa makurutu wa polisi

Jamii wa Ogiek inayoishi katika kaunti ndogo ya Narok kusini inalalamika baada ya mmoja wa vijana wao kuchujwa kwenye shughuli ya kuwasajili makurutu kujiunga na huduma ya taifa ya polisi licha ya kufaulu kwenye zoezi hilo.

Wakiongozwa na Reverend Fred Lemama wa kanisa la Covenant Christian International (CCI), watu wa jamii hiyo walidai kuwa licha ya wao kutengewa nafasi mbili kwenye zoezi hilo, kijana huyo aliuchujwa bila sababu zozote kutolewa.

Lemama alidai kuwa juhudi za kusuluhisha suala hilo na afisa wa usajili hazikufua dafu kwani aliwafukuza.

Kundi hilo lilishangaa kwanini majina ya wawaniaji waliofaulu hayakuchapishwa licha ya wakazi kadhaa kushinikiza kuonyeshwa orodha hiyo.

Kundi hilo lilimuandikia rufaa kamishna wa kaunti ya Narok, Evans Achoki, likiitaka halmashauri huru ya kutathmini utenda kazi wa polisi-IPOA kuchunguza suala hilo.

Tuliwasilisha malalamishi yetu kwa kamishna wa kaunti ndogo Felix Kisalu ambaye alituelekeza kwa kamishna wa kaunti. Tayari tumemwandikia kamishna wa kaunti malalamishi yetu ili awapatie asasi husika,” alisema Lemama

Kwa upande wake, Achoki alisema amepokea malalamishi rasmi kutoka jamii ya Ogiek na amewasilisha malalamishi hayo kwa halmashauri ya IPOA kwa uchunguzi zaidi.

Wanaume 13 na wanawake wawili walifuzu kujiunga na huduma ya taifa ya polisi katika kaunti hiyo ndogo ya Narok Kusini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *