Jaji Amy Coney Barrett aidhinishwa kuwa jaji wa mahakama ya juu Marekani
Bunge la Seneti nchini Marekani limeidhinisha uteuzi wa Jaji Amy Coney Barrett kuwa jaji wa Mahakama ya Juu, hatua ambayo ni ushindi kwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo wiki moja kabla ya uchaguzi wa rais nchini humo.
Maseneta wanachama wa chama cha Rais Trump cha Republican walipiga kura 52 dhidi ya 48 kuimuidhinisha jaji huyo na kuwashinda wapinzani wao wa chama cha Democrat.
Jaji huyo wa umri wa miaka 48 alikula kiapo katika Ikulu ya Whitehouse mbele ya Rais Trump.
Ni seneta mmoja pekee wa chama cha Republican, Susan Collins, ambaye anakabiliwa na ushindani mkali wa uchaguzi huko Maine, aliyepiga kura dhidi ya mteule huyo wa rais Trump katika kura hiyo ya jana jioni.
Jaji Barrett ndiye jaji wa tatu aliyeteuliwa na rais Trump kuhudumu katika mahakama ya juu, baada ya Neil Gorsuch aliyeteuliwa mnamo 2017 na Brett Kavanaugh mnamo 2018.