IPOA kuchunguza mashambulizi ya polisi dhidi ya mwanahabari wa shirika la KBC
Halmashauri ya Kuthathmini Utendaji Kazi wa Kikosi cha Polisi (IPOA) imezindua uchunguzi kuhusu kisa ambacho kilinaswa kwenye kanda video ambapo maafisa wa polisi walionekana kumshambulia mwendeshaji gari mmoja na pia mwanahabari ambaye alinasa kisa hicho katika kaunti ya Nakuru.
Kupitia taarifa, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anne Makori alisema halmashauri hiyo itatoa mapendekezo yanayofaa ya utovu wa nidhamu dhidi ya maafisa hao wa polisi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Huduma ya Polisi ya Kitaifa, Tume ya Huduma ya Polisi ya Kitaifa, au asasi yoyote husika ya Serikali.
Sehemu ya kanda hiyo ya video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha maafisa watatu wa polisi wakimshambulia mwendeshaji gari mmoja ambaye alikuwa akilalamika baada ya mmoja wa maafisa hao wa polisi wa trafiki ambaye alikuwa akidhibiti trafiki katika eneo la Baranabas kugonga gari lake kwa kijiti.
Mwandishi mmoja wa habari wa shirika la Utangazaji Nchini (KBC) wa eneo la Nakuru, Simon Ben aliyerekodi kanda ya ugomvi kati ya maafisa hao na mwendesha gari katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi sasa anauguza majeraha baada ya kushambuliwa na maafisa wa polisi kwa kurekodi kisa hicho.
Alitafuta matibabu katika hospitali kuu ya kaunti ya Nakuru kabla ya kuripoti swala hilo katika kituo kikuu cha polisi cha Nakuru