Ingwe yaichuna Sharks huku KCB wakiwazima Western Stima
AFC Leopards waliwakwaruza Kariobangi Sharks mabao 2-0 katika mchuano wa ligi kuu uliopigwa Jumapili alasiri katika uwanja wa Kasarani.
Elvis Rupia alipachika bao la kwanza dakika ya 11 huku wakiongoza kwa goli hilo kufikia mapumziko.
Kipindi cha pili pande zote zilicheza kwa tahadhari huku wageni Ingwe wakilazimika kumaliza mechi na wachezaji 10 uwnajani kufuatia kupigwa kadi nyekundu kwa Fabrice Mugheni dakika ya 89.
Kadi hiyo nyekundu haikuwatamausha Leopards walioongeza mashambulizi na Jefari Odeny akaongeza bao la pili kunako dakika ya 92 ukiwa ushinde wa pili kwa Sharks msimu huu.
Katika mikwangurano mingine Kakamega Hombeboyz wakiwa nyumbani Bukhungu waliikung’uta Bidco United magoli 2-0 Ali Bhai na Moses Mudavadi wakipachika mabao yote katika kipindi cha kwanza wakati KCB wakiiparuza Western Stima mabao 3-1 katika uga Moi kaunti ya Kisumu.
Kcb wangali kushikilia kukutu uongozi wa ligi hiyo kwa pointi 21 baada ya michuano 8 wakifuatwa na Tusker Fc kwa alama 20 huku Wazito Fc wakifunga orodha ya tatu bora kwa alama 17.