IEBC yazindua rasmi zoezi la uthibitishaji saini za BBI

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imezindua zoezi la kuthibitisha saini zilizokusanywa na kamati ya BBI katika Ukumbi wa Bomas.

Kupitia taarifa, tume hiyo imesema kuwa makarani 400 walioajiriwa kwa ajili ya zoezi hilo wamepokea kiapo cha siri na wataanza mafunzo mara moja.

IEBC pia imeidhinisha watu 72 wanaowakilisha mashirika sita ambao watakuwa waangalizi wa mchakato wa uthibitishaji wa saini hizo.

Wakati uo huo, tume hiyo ya IEBC imewahimiza maafisa wake, makarani na waangalizi wa mchakato huo kuzingatia kanuni za kujiepusha na maambukizi ya COVID-19 kwa ajili ya usalama kwa wote.

“Mahali pa kuthibitisha saini pameandaliwa kwa vifaa vya kutosha vikiwemo vieuzi na sehemu za kunawa mikono ili kuhakikisha kwamba kanuni za usalama kutokana na COVID-19 zinazingatiwa,” imesema IEBC.

Tume hiyo itapokea kitita cha shilingi milioni 93.7 kutoka kwa Wizara ya Fedha ili kufadhili zoezi hilo, huku makarani wakilipwa shilingi 1,200 kila siku.

Awali, tume hiyo ilikuwa imeomba shilingi milioni 241 kwa ajili ya zoezi hilo lakini serikali ikapunguza fedha hizo hadi shilingi milioni 93.7.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *