Idara ya Utabiri wa hali ya hewa yaonya kuhusu mvua kubwa kuanzia Ijumaa

Idara ya Utabiri wa hali ya hewa imeonya kwamba mvua kubwa inatarajiwa siku ya Ijumaa katika maeneo mbali mbali humu nchini.

Idara hiyo imesema maeneo hayo ni pamoja na Magharibi mwa Kenya, Mlima Kenya, Kusini-Mashariki pamoja na Kaskazini-Mashariki mwa nchi.

Kwenye taarifa, idara hiyo imesema mvua hiyo inatarajiwa kuwa ya zaidi ya kiasi cha milimita 20 na huenda ikaendelea siku ya Jumamosi tarehe 23 katika sehemu za nyanda za juu, Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa.

Idara hiyo imeongeza kwamba mvua hiyo huenda ikapungua siku ya Jumapili.

Upepo kutoka Mashariki ukielekea Kusini-Mashariki mwa nchi, unatarajiwa kuvuma kwa mwendo wa zaidi ya mita 12.9 kwa sekunde katika sehemu hizo.

Idara hiyo imewatahadharisha wakazi wa maeneo yaliyotajwa kwamba huenda kukatokea mafuriko hata katika maeneo ambako hapakunyesha mvua kubwa.

Aidha, imewaonya watu dhidi ya kuendesha magari kwenye maji yaliotwaama na pia kutembea kwenye maji hayo, na hata  kujikinga chini ya miti  ili kuepusha kupigwa na radi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *