Idadi ya vifo vilivyotokana na mafuriko nchini Indonesia na Timor yafikia 71

Idadi ya watu walioaga dunia kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyokumba Indonesia na Timor Mashariki hapo jana sasa imefikia watu 71.

Mvua kubwa imesababisha uharibifu mkubwa katika nchi hizo majirani za Kusini Mashariki mwa Bara Asia, huku maji kutoka kwenye mabwawa yaliyofurika yakisomba maelfu ya makazi.

Eneo lililoathirika ni kutoka Kisiwa cha Flores Mashariki ya Indonesia hadi Timor Mashariki.

Zaidi ya watu 40 bado hawajulikani waliko nchini Indonesia, huku maafisa wakionya kwamba idadi ya walioaga dunia huenda ikaongezeka zaidi.

Takriban watu 21 wameaga dunia huko Timor Mashariki, ifahamikayo pia kuwa Timor Leste, kulingana na mashirika ya habari yaliyowanukuu maafisa katika nchi hiyo ya kisiwa.

Waathiriwa wengi wanaaminika kuwa katika jiji kuu Dili.

Rais Joko Widodo wa Indonesia ametoa risala zake za rambirambi na kuwahimiza watu kuzingatia ushauri wa maafisa wakati wa hali duni za anga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *