Huenda serikali ikarejesha baadhi ya masharti ya kudhibiti Covid-19

Katibu mwandamizi katika wizara ya afya Dkt Mercy Mwangangi amesema serikali huenda ikalazimika kurejesha baadhi ya masharti ya kukabiliana na msambao wa Corona, endapo visa vya maambukizi vitaongezeka.

Dkt Mwangagi alisema wizara ya afya itachunguza kiwango cha maambukizi kwa muda wa majuma mawili kabla ya kuamua kuhusu hatua itakazochukua kuzuia maambukizi zaidi.

Akiongea wakati wa mahojiano katika kituo cha KBC Radio Taifa, Dr Mwangangi alipinga dhana kuwa ongezeko la maambukizi ya Corona humu nchini limetokana na wimbi la pili la virusi hivyo.

Alifafanua kuwa hii ingewezekana tu iwapo chamko la kwanza la virusi hivyo lingekabiliwa.

Kulingana na Dkt. Mwangangi, ongezeko la maambukizi limetokana na hali ya Wakenya kupuuza masharti ya kuzuia msambao wa virusi hivyo yaliyowekwa na wizara ya afya.

“Jambo la Corona si la mtu wala serikali, bali ni letu sote kugharamikia na kuliangamiza,” alisema Mwangangi

 

Vile vile alisema idadi hiyo kubwa ya visa vya maambukizi imethibitishwa kutokana na uwezo wa Kenya wa kupima sampuli nyingi wakati huu baada ya kupata vifaa zaidi vya kutekeleza shughuli hiyo.

Kenya Alhamisi ilinakili idadi ya juu zaidi ya visa vya Corona, huku visa 1,068 vikidhibitishwa.

Hii ilifikisha 47,212 idadi ya jumla ya visa vya maambukizi humu nchini. Visa hivyo vipya vilinakiliwa baada ya sampuli 7,556, kupimwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *