Huduma ya taifa kwa vijana NYS, kutoa mafunzo kwa waendeshaji pikipiki kote nchini

Wahudumu milioni 1.4 wa bodaboda wanatarajiwa kupokea mafunzo kuhusu kanuni za barabarani kuanzia wiki ijayo.

Mafunzo hayo yanayotarajiwa kutolewa na huduma ya vijana kwa taifa-NYS kupitia wizara ya teknolojia ya habari na mawasiliano-ICT, yatawezesha asilimia 40 ya wahudumu wasiokuwa na leseni kupata leseni zao za uendeshaji pikipiki.

Waziri wa habari Joe Mucheru alisema wizara hiyo inashirikiana na NYS kutoa mafunzo kwa wahudumu milioni 1.4 kuhusu kanuni za barabara kuu na usalama wa barabarani.

“Tunatarajia kukamilisha mpango huu katika muda wa miezi michache ijayo kuhakikisha waendeshaji wote wa pikipiki wanapata ujuzi unaohitajika sawia na kupata leseni,” alisema Mucheru.

Mucheru alisema kwamba mafunzo hayo yatatolewa kwa kaunti zote 47 kwa gharama ya shilingi 750 kwa mtu mmoja.

Mucheru amesema kiwango hicho ni nafuu kwani waendeshaji pikipiki wengi hawawezi kumudu karo ya vyuo vya uendeshaji pikipiki.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwenyekiti wa baraza la huduma ya vijana kwa taifa, NYS luteni jenerali mstaafu Njuki Mwaniki, alisema mpango huo unanuia kuhakikisha nidhamu na uzingativu wa sheria za trafiki,kuwaelimisha waendeshaji pikipiki mbinu za kurekebisha pikipiki, mafunzo ya huduma ya kwanza na jinsi ya kushughulikia ajali.

“Tunafuraha kutoa mchango wetu kwa waendeshaji boda boda kwani wao ni miongoni mwa mfumo wa uchukuzi wa kitaifa huku wengi wao wakiwa vijana. Mpango huu ambao tunauanzisha utatekelezwa katika maeneo bunge yote kote nchini,” alisema Mwaniki.

Ripoti ya halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani inaonyesha kwamba idadi ya ajali iliongezeka mwaka 2020, kati ya mwezi Januari na Aprili 23 vikiwa visa 1,022 ambapo 107 walikuwa abiria wa pikipiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *