Hotuba ya Rais kuhusu hali ya taifa kutolewa leo

Rais Uhuru Kenyatta leo anatarajiwa kutoa hotuba ya mwaka huu kuhusu hali ya taifa kwenye kikao cha pamoja cha Bunge la Kitaifa na Seneti.

Miongoni mwa maswala mengine, kiongozi wa taifa anatarajiwa kuzungumzia mafanikio ya serikali katika ajenda za maendeleo, miaka miwili baada ya kuchaguliwa kwa awamu ya pili.

Matayarisho yamekuwa yakifanywa bungeni kwa ajili ya maandalizi ya kikao hicho kuambatana na kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona.

Kwenye hotuba hiyo inayosubiriwa kwa hamu, Rais Kenyatta huenda akazungumzia pia hatua zilizopigwa kwenye vita dhidi ya janga la COVID-19, lililodumu kwa takribani miezi saba sasa.

Juhudi za kuleta umoja nchini kupitia mpango wa upatanisho wa kitaifa, BBI, pia huenda zikashamiri katika hotuba hiyo.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na wa Seneti Ken Lusaka waliwaarifu rasmi wabunge kuhusu kikao hicho cha pamoja kupitia chapisho Ijumaa iliyopita.

Kwenye taarifa, Spika Muturi na Lusaka walifichua kwamba Rais angehudhuria kikao hicho cha pamoja siku ya leo kwa hafla hiyo ya kila mwaka.

Miaka iliyopita, Rais alitoa hotuba hiyo kati ya mwezi Machi na Mei kila mwaka isipokuwa mwaka huu ambapo amechelewa kufanya hivyo kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *