Harmonize kushirikiana na msanii Anjella

Je utahisi vipi ikiwa wewe ni mwanamuziki anayeibukia, unajihusisha sana na kurudia nyimbo za wasanii wakubwa alafu siku moja msanii tajika anakuomba ufanye naye muziki?

Ndiyo hadithi ya mwanadada Anjella wa nchi ya Tanzania ambaye anajiita “Anjella_tz” kwenye Instagram.

Konde Boy au ukipenda Harmonize,alipata video ya Anjella akiimba wimbo wa mwanamuziki mwingine wa Bongo kwa jina Aslay, ikamfurahisha akaiweka kwenye akaunti yake ya Instagram akiomba aunganishwe naye.

Alipomfahamu, alimtumia ujumbe wa kuomba afanye naye kazi. Mara ya kwanza Anjella hakuamini lakini baadaye aliitikia wito na punde baada ya Harmonize kurejea Tanzania kutoka Ghana, walikutana na kuweka mikakati ya ushirikiano wao.

Harmonize ametangaza kwamba wimbo wake wa kwanza mwaka huu utakuwa huo ushirikiano kati yake na Anjella ambaye ana tatizo la kuvimbiwa miguu.

Mwanamuziki huyo wa Tanzania anayemiliki kampuni ya muziki kwa jina Konde Gang, huenda akaishia kumsajili Anjella kwenye kundi lake la wanamuziki.

Harmonize ametangaza kwamba wimbo huo wake na Anjella utazinduliwa rasmi tarehe ishirini, mwezi huu wa Januari mwaka 2021.

Tayari Harmonize ameanza kumtafutia Anjella mwanamitindo ambaye atamsaidia kubadili muonekano wake anapoanza kupaa katika fani ya muziki huku akimshukuru kwa kukubali kufanya kazi ya muziki naye.

Ikiwa atasajiliwa kwenye Konde Music, Anjella atakuwa msanii wa kwanza wa kike chini ya usimamizi wa Harmonize ambaye alitoka WCB.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *