Categories
Burudani

Harmonize amtambua Diamond Platnumz

Mwanamuziki wa Tanzania kwa jina Harmonize amechagua kumtambua mwanamuziki mwenza Diamond Platnumz katika kheri njema za mwaka mpya.

Wanamuziki hao wawili wa Tanzania wanasemekana kutokuwa na uhusiano mzuri hasa baada ya Harmonize kugura kampuni ya muziki kwa jina Wasafi Classic Baby – WCB inayomilikiwa na Diamond.

Mmiliki huyo wa Konde Music amewashangaza wengi baada ya kuamua kumtambua rafiki yake wa zamani ambaye pia alikuwa mkubwa wake.

Aliweka picha ya Diamond Platnumz kwenye akaunti yake ya Instagram na kuandika, “Nazungumza kutoka moyoni naakupenda kakangu. Ni mwaka mpya 2021. Asante kwa kubadilisha maisha yangu. wewe pekee uliona dhahabu kwenye mchanga na giza jingi sana!!! Leo hii Afrika nzima na hasa Afrika Mashariki wanajivunia uwepo wangu. Upendo huu ni wa milele ndugu yangu. Kila nilichokifanya nilikuwa na nia ya kukufurahisha usinielewe vibaya. Keti peke yako bila yeyote pembeni usome ujumbe huu utaelewa ninachomaanisha. Wewe ni shujaa. wakati mwema. Mimi Konde Boy na wanamuziki wote wa Konde Gang tunakupenda. Mwaka mpya mwema Chibu Dangote Diamond Platnumz kaka mkubwa.”

Haya yanajiri baada ya Harmonize kujaribu kuonyesha kwamba kuna uhasimu kati yake na Diamond kupitia wimbo alioutoa mwisho wa mwaka jana kwa jina “Ushamba”.

Alionekana kumkejeli Diamond kwenye wimbo huo na alipohojiwa, Diamond alisema ushindani ni muhimu katika sekta ya muziki nchini Tanzania ili isonge mbele.

Harmonize ameandika maneno hayo usiku wa kuamkia leo na anaonekana kana kwamba bado yuko nchini Ghana ambako alikuwa amekwenda kwa likizo.

Diamond Platnumz hajajibu hatua hii ya mkono wa maridhiano kutoka kwa Harmonize, anaonekana kuzamia kazi ambapo jana yeye na kikosi kizima cha Wasafi media walikuwa katika eneo la Dodoma kwa ajili ya ile ziara yao kwa jina “Tumewasha na Tigo”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *