Hali ya taharuki yatanda Jijini Mogadishu

Makabiliano makali yameripotiwa kwenye mji mkuu wa Somalia wa Mogadishu,huku kundi moja la viongozi wa upinzani likikaidi marufuku ya mikutano ya umma na kufanya maandamano.

Vyama vya upinzani vimemtaka Rais Mohamed Abdullahi Farmajo kung’atuka baada ya muda wake wa kuhudumu kukamilika wiki jana.

Duru zinasema kuwa  mgombeaji wa urais wa upinzani Abdirahman Abdishaku,alikuwa miongoni mwa waliojaribu kuandamana.

Hali hiyo ya wasi wasi ilisababisha safari za kimataifa kusitishwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden Adde uliopo Jijini Mogadishu.

Maafisa wa usalama walifyetua risasi angani kuwatawanya wandamanaji.

Aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Hassan Ali Kheyre amedai kupitia mtandao wa Facebook kuwa amenusurika jaribio la kumuua.

Rais wa Zamani wa Somalia Hassan Sheikh alilaumu utawala wa Farmajo kwa kuwashambulia raia wasiokuwa na hatia akisema kile raia wanafanya ni maandamano ya amani.

Maandamano hayo yamesababishwa na hatua ya taifa hilo kutoandaa uchaguzi mkuu huku muhula wa Rais Mohamed Abdullahi Farmajo wa miaka minne ulikamilika Februari 8.

Makundi ya upinzani yamekuwa yakitoa wito ajiuzulu, ingawa serikali imesema kuwa rais atasalia madarakani hadi utawala mpya utakapochaguliwa.

Hata hivyo hakuna tarehe iliyowekwa ya kufanya kwa uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *