Haji ataka kuchunguzwa kwa ghasia zilizoghubika chaguzi ndogo za Alhamisi

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji amemuagiza Inspekta Jenerali wa polisi Hilary Mutyambai kuanzisha mara moja uchunguzi wa pamoja kwenye madai ya ghasia na maovu mengine ya uchaguzi katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Matungu lililoko kaunti ya kakamega na wadi ya London katika kaunti ya Nakuru.

Mkurugenzi huyo wa mashtaka ya amemuagiza Inspekta Jenerali wa polisi kuwasilisha faili ya uchunguzi huo afisini mwake katika muda wa siku thalathini.

Kwenye barua ya pili,mkurugenzi wa mashtaka ya umma amemuagiza Mutyambai,aanzishe uchunguzi wa kuthibitisha video inayosambazwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inayomuonyesha mtu anayeshukiwa kuwa aliyekuwa waziri Rashid Echesa akimzaba kofi afisa wa tume huru ya uchaguzi na mipaka katika eneo bunge la Matungu.

Kupitia kwa taarifa siku ya Jumamosi tume ya uchaguzi na mipaka humu nchini IEBC, ilikashifu visa vya ghasia vilivyoshuhudiwa katika chaguzi ndogo za siku ya Alhamisi ikisema visa kama hivyo hakitakubalika katika uchaguzi mdogo wa kiti cha useneta kaunti ya Machakos.

Waziri wa zamani wa michezo Rashid Echesa alitiwa nguvuni siku ya Ijumaa jioni kwa kumzaba kofi afisa wa IEBC Peter Okura katika kituo cha kupiga kura cha shule ya msingi ya Bulonga siku ya Alhamisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *