Categories
Michezo

Gor na Wazito FC wafungiwa kusajili wachezaji kwa mwaka mmoja kwa kushindwa kuwalipa wachezaji

ShirikIsho la soka ulimwenguni FIFA   limezipiga marufuku timu za  Gor Mahia  na  Wazito Fc kusaini wachezaji wapya kuanzia msimu huu  wa uhamisho wachezaji kwa kushindwa kuwalipa wachezaji  Dickson Ambudo na   Augustin Otu  mtawalia.

Yamkini gor walishindwa kumlipa wing’a wa Tanzania Ambudo shilingi milioni 1 nukta 2 alipowachezea  yakiwa malimbikizi ya mshahara na marupurupu huku Wazito wakikosa kumlipa  Otu kutoka Liberia shilingi milioni 1 baada ya kukatiza kandarasi yake kwa njia isiyofaa kinyume na kandarasi.

Ambudo na  Otu walikuwa wamewasilisha kesi yao kwa jopo la kutatua mizozo kwenye shirikisho la FIFA  disemba 16 na 26 mtawalia.

Vilabu hivyo vilipewa makataa ya siku 45 kuwalipa wachezaji hao au vipigwe marufuku .

Hata hivyo inasubiriwa kuona hatua ambayo FKF itazichukulia timu hizo mbili kwani kogalo walikuwa wamekamilisha usajili wa mshmabulizi wa Brazil Wilson Silva Fonseca, nahodha wa zamani Harun Shakava  na  Abdul Karim Nikiema Zoko  kutoka Burkina Fasso kwa kandarasi ya miaka miwili kila mmoja.

Upande mwingine , Wazito walimsajili kiungo wa Sopaka  Eli Asieche.

Endapo zitawalipa wachezaji hao ,timu hizo mbili ziko huru kusajili wachezaji wapya kuanzia Agosti mwaka ujao.

Ambudo,ambaye kwa sasa anachezea timu ya  Dodoma Jiji  katika ligi kuu ya Tanzania bara aliondoka Gor Julai mwaka jana baada ya kukamilika kwa mkataba wake  wa mkopo wakati Otu akiwa kati ya wanandinga 12 waliotimuliwa na usimamizi wa Wazito Fc Julai mwaka jana.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *