Gor na Wazito FC wafungiwa kusajili wachezaji kwa mwaka mmoja kwa kushindwa kuwalipa wachezaji
ShirikIsho la soka ulimwenguni FIFA limezipiga marufuku timu za Gor Mahia na Wazito Fc kusaini wachezaji wapya kuanzia msimu huu wa uhamisho wachezaji kwa kushindwa kuwalipa wachezaji Dickson Ambudo na Augustin Otu mtawalia.
Yamkini gor walishindwa kumlipa wing’a wa Tanzania Ambudo shilingi milioni 1 nukta 2 alipowachezea yakiwa malimbikizi ya mshahara na marupurupu huku Wazito wakikosa kumlipa Otu kutoka Liberia shilingi milioni 1 baada ya kukatiza kandarasi yake kwa njia isiyofaa kinyume na kandarasi.
Ambudo na Otu walikuwa wamewasilisha kesi yao kwa jopo la kutatua mizozo kwenye shirikisho la FIFA disemba 16 na 26 mtawalia.
Vilabu hivyo vilipewa makataa ya siku 45 kuwalipa wachezaji hao au vipigwe marufuku .
Hata hivyo inasubiriwa kuona hatua ambayo FKF itazichukulia timu hizo mbili kwani kogalo walikuwa wamekamilisha usajili wa mshmabulizi wa Brazil Wilson Silva Fonseca, nahodha wa zamani Harun Shakava na Abdul Karim Nikiema Zoko kutoka Burkina Fasso kwa kandarasi ya miaka miwili kila mmoja.
Upande mwingine , Wazito walimsajili kiungo wa Sopaka Eli Asieche.
Endapo zitawalipa wachezaji hao ,timu hizo mbili ziko huru kusajili wachezaji wapya kuanzia Agosti mwaka ujao.
Ambudo,ambaye kwa sasa anachezea timu ya Dodoma Jiji katika ligi kuu ya Tanzania bara aliondoka Gor Julai mwaka jana baada ya kukamilika kwa mkataba wake wa mkopo wakati Otu akiwa kati ya wanandinga 12 waliotimuliwa na usimamizi wa Wazito Fc Julai mwaka jana.