Gor Mahia yampiga marufuku katibu mkuu Sam Ochola kwa ‘kuuza timu’
Kilabu cha Gor Mahia kimempiga marufuku katibu mkuu wake Sam Ocholla kwa kusaini barua ya mkataba wa kupeperusha mechi la ligi kuu FKF baina ya kampuni ya Star Time na FKF.
Akitangaza kumpiga marufuku ya Ocholla,mwenyekiti wa Gor Ambrose Rachier amesema kuwa ilikuwa kinyume cha sheria kwa katibu huyo kusaini barua hiyo bila kushauri usimamizi mkuu wa timu na tayari wameandika barua kwa kampuni ya Stars Times kujitenga na mwafaka huo.
Kulingana na Rachier uamuzi huo sio wa kuchukuliwa na mtu binafsi.
“kulingana na katiba ya kilabu ibara ya 15 mkataba wowote kama huo unaweza ukatiwa saini tu mwenyekiti wa timu,na hatuko tayari kuuza haki zetu kwa huo mkataba kwani hatujaona kandarasi kati ya FKF na Stars Times ndio maana hatukubaliani na mkataba huo”akasema Rachier
Rachier amesisitiza kuwa wako tayari kushiriki ligi kuu inayotazamiwa kuanza tarehe 28 mwezi huu,lakini hawatauza haki zao kwa kusaini mkataba huo.
”Sisi tuko tayari kaunza ligi lakini kile hatutafanya ni kuuza haki zetu,kile FKF wanafanya ni kinyume cha sheria kwa vilabu kupokonywa haki zao”akaongeza Rachier
Hata hivyo Ochola ameitisha kikao na wanahabari Jumatano kujitetea akidokeza kuwa uamuzi huo wa kusaini barua ya mkataba aliuafikia baada ya kupewa idhini na baraza kuu la kilabu.
Kampuni ya Star Times yenye makao yake nchini China ilisaini mkataba wa miaka 7 na Fkf kumiliki haki zote za matangazo ya runinga ya ligi kuu ,mechi za timu za taifa za wanaume na wanawake na mechi 30 za ligi ya NSL.
Vilabu vinne vimedinda kusaini mkataba huo vikiwemo Gor Mahia,Ulinzi Stars ,Mathare United na Zoo Fc kwa misingi ya kutofahamu yaliyimo kwenye kandarasi hiyo.